Friday, August 28, 2009


Uchaguzi CCM msimamizi akimbia na majina

Katika Kata ya Manzese hapa jijini Dar es Salaam kasi ya vurumahi ilipamba moto baada ya kuzagaa uvumi kuwa kuna wanachama feki wamejitokeza kupiga kura huku wengine wakidai kuwa kuna vigogo (waliowaita mafisadi) wameingia katika kumbi za kupigia kura wakiwa na majina feki kwa lengo la kuhakikisha mlengwa wao anashinda.

Wengi wa Wanachama wamedai kusikitishwa na ujanjaujanja uliokuwa unaendelea na kuwatia wasiwasi uliozua maswali mengi yasiyo na majibu. Wamedai kuwepo kwa hujuma nyingi tangu kwenye kuunga foleni na zoezi lilikuwa na utata.

Baadhi ya viongozi wakizungumzia hali hiyo bila kutaja majina yao wamedai kuwa kuna kundi la vijana wa kihuni waliopandikizwa (mamluki) kuleta fujo katika zoezi hilo.

Pia kiongozi mmoja msimamizi ambaye jina lake halikujulikana mara moja ameripotiwa kubeba orodha ya wanachama wa kituo chake na kukimbia nayo kusikojulikana huku akidai kuwepo watu wengi waliomtia wasiwasi ambao amesema si wanachama.

Kadi nyingi za wanachama zimechanwa kwa hasira kutupwa tupwa barabarani huku pia watu wengi wakijeruhiwa katika vurumahi hiyo ikiwa ni pamoja na viongozi wao kama ilivyokuwa kwa Mjumbe wa Tawi la Mvuleni Ramadhani Msumi. Shughuli hiyo imekuwa pevu na hakieleweki nini kitaendelea hapo kesho kutokana na kuwepo kwa hali ya kutokuelewana huku kila mmoja akionekana kama adui kwa mwenzake.

No comments:

Post a Comment