Friday, October 15, 2010

Kutochanganya dini na siasa viongozi wapangiwe mahubiri?

Na Joseph Sabinus,
silas_mbise@yahoo.com

OKTOBA 31, mwaka huu Tanzania inafanya zoezi kubwa na linalokodolewa macho na mataifa mengine, hasa wenye nia mbaya na taifa hili wakisubiri kwa uchu Watanzania wafanye kosa, ili walitumie hili kuja kuwatawala iwe kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na hata kiulinzi.


Ndiyo; wapo wanaolisubiri hilo na huku wakiliweka taifa katika mzani ili wapime busara za Watanzania kuona kama wanadanganyika, au hawadanganyiki.
Hapana siri, mara nyingi nimekuwa nikisisitiza katika makala zangu kuwa, popote duniani, machafuko mengi katika mataifa hutokana ama kwa sababu za kisiasa, au za kidini.
Ni kwa msingi huo, kumekuwapo na dhana mbalimbali miongoni mwa watu wakitaka viongozi wa dini, waepuke kuwagawa waamini wao kwa kuonesha ushabiki wa kisiasa dhidi ya vyama vya kisiasa vinavyoshindana. Hilo halina ugomvi.

Kutokana na hadhari hii inayotokana na ukweli kuwa viongozi wa dini wana wafuasi kutoka katika vyama mbalimbali na tofauti, kumekuwa na mahusiano ya “mwisho wa mwezi” baiana ya baadhi ya viongozi wa wanasiasa na viongozi wa dini.
Mara kadhaa Serikali kupitia wasemaji wake mbalimbali, imekuwa ikiwatumia viongozi wa dini na hata kuwaomba kuwahamasisha waamini kushiriki mambo mbalimbali yakiwamo kujitokeza katika kujiandikisha katika sense ya taifa, kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, kushiriki harakati za kampeni kistaarabu na pia, kubwa zaidi kushiriki katika tukio la kupiga kura siku inapowadia.
Viongozi wa dini wanapolifanya hawapaswi kuombwa wala kupongezwa kwani ninaamini kuwa, ni sehemu ya majukumu yao. Nasema hivyo kwani kwangu mimi, ninaamini viongozi wa dini tofauti na viongozi wa kisiasa wanaolea watu kimwili, wao (viongozi wa dini) wanalea watu kiroho na kimwili.
Kumlea mwanadamu kiroho kwa mujibu wa uelewa wangu ni kumjenga katika misingi inayomuwezesha kupokea neema za Mungu kwa kadiri ya mawazo, maneno na matendo yake mema yanayoondana na mapenzi ya Mungu.

Wakati huo, kumlea mwanadamu kimwili, ni harakati za kumtengeneza mwanadamu huyu huyu apate mahitaji, haki na wajibu wake kama mwanadamu. Hili linapofanyika, linakuwa kichocheo kikubwa cha watu kulelewa na kuishi vyema kiroho.
Hii inatokana na ukweli kuwa, binadamu sio tu mwili, au basi roho pekee, bali vyote moja; mwili na roho.
Kitendo cha baadhi ya wanasiasa kupenda kusifiwa na kualikwa katika matukio mbalimbali ya kidini ili wapate nafasi za kuhutubia na kujulikana kwa nyadhifa zao, lakini hao hao wakawa wa kwanza kuwakosea adabu viongozi wa dini wanapokemea maovu yanayofanywa na wanasiasa, ni jambo lisilopaswa kufanywa na mwenye akili timamu.

Ninasema hivyo kwani nakumbuka tangu maandalizi ya awali ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaofanyika mwishoni mwa mwezi huu yaanze, viongozi mbalimbali wa kidini wamekuwa wakijitahidi kutumia nafasi zao kutoa elimu ya uraia kwa waamini wao.

Kinachoshangaza, viongozi hao wanapotimiza wajibu huo wa msingi, ikiwa ni pamoja na kuelezea sifa za kiongozi bora anayestahili kuchaguliwa au wanapotaja baadhi ya mambo yasiyopaswa kutumika kumpata kiongozi mfano, uchama, udini, ukabila na mengine ya namna hiyo, wanaambiwa wamechanganya dini na siasa.

Wanasiasa hao wanashindwa kujulikana kama wao ni popo, au ni ndege maana wako mguu mmoja ndani, wakisikia mambo yanayowapamba, wanakaa kimya na kutikisa vichwa ishara ya kuunga mkono mahubiri au mafundisho yaliyotolewa, lakini mahubiri yanapowagonga, wanakuwa wa kwanza kupaza sauti na kuwakaripia viongozi wa dini kuwa wanachanganya dini na siasa.
Baaadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria Mkutano wa pamoja wa viongozi wa dini, viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa, wanahabari, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wawakilishi wa asasi za kiraia, walikuwa miongoni mwa watu wanaokaribia “kuwanyooshea wenzao vidole eti wanakosea kutoa mahubiri au mafundisho ya elimu ya uraia.”

Inashangaza! Inashangaza tena inashangaza sana kuona kuwa adui wa mtu ni mtu mwenyewe. Inafikia hatua mtu akaamini kuwa, baaadhi ya viongozi wa dini tena wachache sana, hawatumiki kwa manufaa ya umma mzima, bali kwa manufaa ya baadhi ya vikundi vya siasa.


Tangu mchakato huu uanze kwa mfano, sijawahi kumsikia kiongozi hata mmoja wa kisiasa akiawaagiza waamini kumchagua mgombea wa chama chochote na katika ngazi yoyote. Nimekuwa nikiwasikia viongozi hao wakizitaja sifa za kiongozi mwadilifu, anayestahili kuchaguliwa kwa maendeleo na ustawi wa watu.
Acheni Munguaitwe Mungu; ukweli ubaki ukweli. Wanasiasa wanaojua wanaguswa na ukweli huo, wanaingiwa hofu na kuanza uzushi kuwa viongozi wa dini waingilia na kuchanganya dini na siasa kwa kumkampenia mgombea wa chama kimojawapo.

Bahati mbaya sana, baadhi ya viongozi wa dini ni kama vile “walikwishanyeshwa sumu” wana masikio, lakini hawasikii, wana macho lakini hawaoni kwamba “wanakubali kufungiwa ndani ya chupa.”
Naukumbuka usemi kuwa, ukitaka kuwatawala watu vizuri, basi wagawe kwanza. Hilo ndilo linalofanyika. Baadhi ya viongozi wa dini, wamelishwa sumu kiasi kwamba hata wanapokuwa wanawakemea wengine kuwa wanachanganya dini na siasa kwa kumpigia debe mgombea wa chama fulani, wakati huo wao wanakuwa wanampigia debe mgombea mwingine.

Inashangaza! Inashangaza sana kama kwa hili, viongozi wa dini ambao wangesimamia ukweli na haki, nao wanageuka na kutaka kuwanyooshea wenzao vidole. Hawa, hapana shaka kuwa hawajui siasa inaanzia wapi na kuishia wapi.
Ni bahati mbaya kuwa, viongozi nao wamekubalishwa kuwa, “wafungiwe ndani” ya misikiti na makanisa. Wasiseme baya linalofanywa na Serikali wala wanasiasa. Kwamba, lolote baya lifanyike kwa watu wao, wao wanyamaze tu, waishie kusema “Yesu alikwenda Yerusalemu” au basi, “Mtume Mohammad alikwenda Makka” Hilo ndilo libaki pekee!


Hapana! Watanzania na hasa wanasiasa; waache viongozi wa dini wafanye kazi zao. Wafanye kazi ya kuwatunza kondoo wao kiroho na kimwili. Wawajibike kutoa elimu ya uraia kwa waamini wao bila kuwekewa mipaka isiyo na kichwa wala miguu.
Inapofikia hatua kiongozi wa dini akavuka mipaka na kuwaamuru waamini wake kumchagua mgombea fulani, basi kwa vile kuna ushahidi, achukuliwe hatua za kisheria maana kama ni elimu, tayari imekwishatolewa; vinginevyo, wasinyimwe uhuru na haki ya kufanya kazi yao ya kuchunga kondoo kiroho na kimwili.

Viongozi wa dini waepuke kuwa watumishi wa baadhi ya wanasiasa na vyama vyao. Waepuke kunyoosheana vidole ili yale yaliyowahi kutokea kwa Askofu Zachary Kakobe wa Full Gospel Bible Fellowship, yasitokee maana mwenzio akinyolewa, wewe tia maji.
Ninakumbuka namna Kakobe alivyowahi kuwakosea heshima Maaskofu wa Kanisa Katoliki kutokana na kile kilichoitwa, Waraka wa Wakatoliki. Kakobe bila kujua kuwa chapisho lile lilitolewa na Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT), akaitisha vyombo vya habari kuwashambulisa Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania.
Kama vile Waswahili walivyowahi kusema kuwa, “Mwosha huoshwa”, kwa kauli yake Kakobe, nayo imechakachuliwa na kuonekana amempigia debe mgombea wa chama fulani. Wakati hilo linafanyika, baadhi ya viongozi wenzake, nao hawako nyuma kumlaumu japo hakutaja jina la mtu wala kuelekeza aliposema, maisha binafsi sio suala muhimu kuangalia katika uchaguzi.
Ndiyo maana katika mkutano huo wa wa juzi katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay Dar es Salaam, Askofu Elias Chessa wa FPCT, alishindwa kuvumilia unafiki. Akasema, “Kuhusu elimu ya mpiga kura, viongozi wa dini tuwe wakweli na Serikali ituamini.”

Akaongeza, “sidhani kama ni dhambi kiongozi wa dini kuwambia waamini wake kwamba tunahitaji kiongozi mwadilifu, kinyume chake jamani, tusiwe wanafiki.”
Akasisitiza ukweli kuwa, jamii inapozungumzia amani, utulivu na usalama kabla, wakati na baada ya uchaguzi, haina budi kuzingatia ukweli kuwa amani ni zao la haki. Kwamba, hata jamii ikiambiwa kuwa ijiandae kupokea matokeo yoyote ya uchaguzi yaani utayari wa kushinda au kushindwa, kama haki haikuendeka na kuonekana imetendeka, ni vigumu kueleweka.”

Kipindi hiki ni muhimu kwa viongozi wa dini wote, kutenda kile kilicho ndani ya mioyo yao wakiamini na kuheshimu ukweli kuwa, wanamwakilisha Mungu hapa duniani. Binafsi katika kikao hicho, nilitegemea viongozi wote wangeshika msimamo wa kuhubiri amani, usalama, utulivu na upendo miongoni mwa jamii, lakini wakati huo huo, waendelee kusema ukweli kama ulivyo hasa pale ambapo kwa busara zao za kichungaji, wanaamini ukweli huo hautaleta madhara.

Ndiyo maana ninaungana na Askofu Dk. Mathew Byamungu wa PCT aliyetoa wito waamini kumchagua kiongozi mwenye kuthamini na kutanguliza utaifa na sio uchama, udini wala ukabila.
Akasema, lazima kuwawepo uvumilivu na upendo miongoni mwa vyama vyote vya siasa kwani, chama kilichopo madarakani, kinaweza kuendelea kuwa madarakani kwa kadiri ya wapigaji kura na pia, chama cha upinzani, kinaweza kuwa chama tawala maana upinzani au utawala haukuumbwa kwa ajili ya mtu au kikundi kimoja.

Mfano mwingine mzuri, niliouona ni angalizo alilolitoa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Anthony Makunde, aliyetaka kila mmoja kwa nafasi yake, awe makini kuhakikisha kwamba, tamko analolitoa linakuwa chachu ya maendeleo ya amani, usalama na utulivu nchini na sio kichocheo cha machafuko.
Ikumbukwe kuwa, viongozi wa dini wasipokuwa makini na wazalendo wanaolipenda taifa lao kwa kumtumikia Mungu kiaminifu, ipo hatari ikajirudia hali ile ambayo baada ya kile kilichoitwa Waraka wa Wakatoliki, Serikali ilipendekeza bungeni kuwa viongozi wa dini wanapotaka kutoa miongozo ya mambo nyeti kama hayo, washauriane na Serikali.

Ninampongeza na kumuunga mkono Akofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwani hakuwa mnafiki alikataa katakata kuwa, haiwezekani kupangiana na kuitisha vikao vya kujadili nini cha kuhubiri au kuwafundisha waamini. Huo ulikuwa msimamo bora wa kichungaji.

Ndiyo maana ninasema, bila kuwa makini na kila kiongozi wa dini kuwa mkweli mbele ya Mungu, basi ipo hatari viongozi wa dini mkajikuta mnaomba wanasiasa wawapangie mambo ya kuhubiri. Hilo likitokea, watakuja hata kuwasaidia kuhubiri kanisani mambo ya siasa; kwa hilo, hawatasema wanachanganya siasa na dini. Kwao, kuchanganya dini na siasa ni kosa, lakini kuchanganya siasa na dini sio kosa.
Tumuombe Mungu atuhurumie, atusaidie na atubariki ili kila mmoja ajitambue kuwa kulinda amani, usalama na utulivu wakati, kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010, ni wajibu wa kila Mtanzania

No comments:

Post a Comment