skip to main |
skip to sidebar
Kutoka Gazeti la Habari Leo
Wazungu ‘waiba’ mamilioni ATM
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata raia wawili wa Bulgaria wanaodaiwa kuiba zaidi ya sh milioni 70 katika mashine za kutolea fedha, ATM jijini Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao, Nedko Stanchen(34) na Stella Nedekcheva(23) walikamatwa mwishoni mwa wiki jijini humo baada ya polisi kuweka mtego wakishirikiana na benki ya Barclays wilayani Kinondoni.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova amesema leo kuwa, vijana hao wanadaiwa kuhusika katika mtandao wa wizi wa fedha katika mashine za ATM za benki mbalimbali.
Amesema, polisi waliweka mtego baada ya mfanyakazi wa benki ya Barclays kugundua kuwa kuna vifaaa vilikuwa vimewekwa katika mashine za ATM.
Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, mfanyakazi huyo alikuwa anafanya usafi, na kwa mujibu wa Kova, vifaa vilivyowekwa kwenye mashine za ATM ni kamera na kifaa cha kunakili taarifa za wateja zilizomo kwenye kadi za ATM.
Wabunge wataka TTCL ilipwe madeni
WABUNGE wameitaka serikali kuilipa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) deni lake la Sh bilioni 9.2 inazodai wizara na taasisi za umma. Wamesema sasa hivi TTCL inakabiliwa na ukata wa fedha, hivyo serikali ilipe deni lake hilo ambalo ni la hadi Juni 2005 na riba na kuisaidia kampuni hiyo kujikwamua kutokana na hali hiyo ngumu.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Ephraim Madeje kwa niaba ya Mwenyekiti wake, Mohamed Missanga, alisema mbali na deni hilo, pia serikali iinusuru kampuni hiyo kwa kulipa madeni yake yote mapema .
Mionzi yadaiwa kuvunja ndoa, kuua paka Mererani
ZAIDI ya wafanyakazi 700 wa mgodi wa kuzalisha madini ya vito vya tanzanite, unaomilikiwa na Kampuni ya Tanzanite One, uliopo Arusha wanadaiwa kuathirika na mionzi iliyotokana na mashine ya X-ray ya kuwakagua iliyopo mgodini hapo.
Baadhi ya waathirika hao wamedaiwa kupata matatizo sehemu za siri na kusababisha kuachwa na wake zao. Tuhuma hizo nzito dhidi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na wawekezaji wa Afrika Kusini, zilitolewa jana bungeni na Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
“Mashine hiyo pia ilishawahi kupitishwa paka, akafa hapohapo kutokana na ukali wa mionzi yake...hili ni tatizo tena wanaopitishwa ni wafanyakazi Waswahili (Watanzania) na Wazungu hawapitishwi”
Gazeti la Mwananchi Leo.
Makachero wamfuata dalali wa Rada
HATIMAYE Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba amezungumzia taarifa za kukamatwa kwa dalali anayetuhumiwa kufanikisha kashfa ya ununuzi wa rada, huku kukiwa na taarifa kuwa wapelelezi wa Tanzania wako Uingereza kufuatilia taratibu za kumrejesha nchini.
Manumba amekuwa akichelea kuzungumzia taarifa za kufuatiliwa kwa mtuhumiwa huyo, Sailesh Vithlan anayedaiwa kufanikisha ununuzi huo tata wa rada yenye thamani ya pauni 28 milioni, lakini jana alidokeza kuhusu uwezekano wa mtuhumiwa huyo kurejeshwa nchini.
“Huwezi kusema ataletwa lini, kinachofanyika ni taratibu za kisheria siyo rahisi kusema lini kwani pia kuna taratibu za kimahakama,� alifafanua Kamishna Manumba alipoulizwa kwamba Vithlan atarejeshwa lini.
Manumba alifafanua kuwa katika kushughulikia suala la mtuhumiwa huyo halina budi kuna ulazima wa kuangalia taratibu nyingine za kisheria, ikiwa ni pamoja na za kimahakama.
Polisi wabaini wizi mkubwa kwenye ATM
WIMBI la wizi wa fedha kwenye akaunti za wateja kupitia mashine za ATM sasa umefikia kiwango cha kutisha baada ya polisi kukamata watu wawili raia wa Bulgaria waliokuwa wanatumia chombo maalumu kunasa namba za siri za kadi na kuchota fedha kirahisi.
Jeshi la Polisi, Kanda ya Dar es Salaam limesema watu hao wanatuhumiwa kuchota kiasi cha Sh70 milioni kutoka kwenye akaunti za wateja wa benki mbalimbali ambao huchukua fedha zao kwenye mashine hizo za ATM.
Kwa mujibu wa polisi, kifaa hicho kina uwezo wa kunakili taarifa za kadi za ATM, ikiwa ni pamoja na namba za siri ambazo huwawezesha wezi kuingia kwenye mashine na kuchota kiasi cha juu cha fedha kulingana na kiwango cha ukomo wa mashine hizo.
No comments:
Post a Comment