Wednesday, June 9, 2010

Oliver Ngoma afariki dunia
MWANAMUZIKI mahiri wa kimataifa, Oliver Ngoma, ambaye ni raia wa Gabon, amefariki dunia juzi usiku akiwa amelazwa hospitalini akisumbuliwa na maradhi ya figo.
Oliver aliyezaliwa Machi 23, mwaka 1959 na kuanza muziki akiwa na umri wa miaka nane tu, atabaki akikumbukwa na wapenzi na mashabiki wa muziki si Gabon na Afrika tu , bali duniani kote.


Kutokana na mchango wake katika medani ya usanii, kamwe hatasahaulika kutokana na kipaji chake cha hali ya juu katika muziki wa Zouk, Rhumba na Reggae huku akijaaliwa uwezo mkubwa wa kucharaza gitaa.


Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Oliver alianza kujihusisha na masuala ya muziki akifuata nyayo za baba yake, aliyekuwa mwalimu wa ala za muziki.


Kipaji chake kilianzia katika bendi ya shule Capo Sound, nchini Gabon alipokuwa akisomea taaluma ya uhasibu.


Kutokana na uhodari wake, Oliver alipewa ufadhili wa masomo katika fani ya uandishi wa habari na kupiga picha nchini Ufaransa.


Oliver ambaye wakati huo alivuma kwa jina la utani la Noli, kati ya vibao vilivyompatia umaarufu ni kile cha Bane alichokitunga mwaka 1989 na kuchezwa katika nchi mbalimbali Afrika na Ulaya.

No comments:

Post a Comment