Mkutano wa Kampeni Peramiho
JK: Hatuwezi Kutoa Huduma za Jamii Bure!
Jakaya Mrisho Kikwete akimnadi mgombea ubunge jimbo la Peramiho Jenister Mhagama wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata mpya ya Mtyangimbole, jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma jana mchana
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali haina uwezo wa kutoa huduma za jamii bure na amewashangaa wanasiasa wanaopita wakiwadanganya wananchi kuwa iwapo wakichaguliwa watatoa huduma hizo bure.
Aliyasema hayo katika kata mpya ya Mchangimbore jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma katika siku yake ya pili ya kampeni katika mkoa huo.
Kikwete alisema serikali ilishajaribu sera hiyo ya huduma bure lakini ilishindwa kwani bidhaa ziliadimika na huduma nyingi zilishindwa kutolewa.
Alisema licha ya maendeleo yaliyofikiwa tangu Uhuru, Tanzania bado ni nchi maskini na haiwezi kutoa huduma bure kama baadhi ya watu wanavyowaahidi wananchi katika kampeni zao.
“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu sana hiyo sera ya bure tulijaribu na ikatushinda na wakati huo hayati baba wa Taifa, Julius Nyerere akiwa mwenyekiti wa chama, tulikaa naye tukaona hilo haiwezekani tukaamua tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure,” alisema Kikwete.


No comments:
Post a Comment