TAMKO LA TAHLISO KWA UMMA KUTAARIFU JUU YA UPOTOSHWAJI
WA HABARI ZINAZOHUSU UPIGAJI WA KURA KWA WANAFUNZI WA
VYUO VYA ELIMU YA JUU TANZANIA.
UTANGULIZI:
TAHLISO ni umoja huru wa wanafunzi, wa Vyuo vya Elimuya ya Juu Tanzania na umoja huu ulianzishwa na kusajiliwa rasmi tarehe 5/5/2004 na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi na namba ya usajili wake ni SO No. 14245 ina wanachama wapatao 53 (Vyuo). Hivi karibuni mjumbe wake mmoja ambaye ni Mwenyekiti wa TAHLISO ametoa taarifa katika vyombo vya habari kuhusiana na suala la upigaji wa kura kwa wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania. Na hivyo basi suala hili kuchukua kasi katika vyombo vya habari kila siku.TAHLISO inasema ndugu Katongo amezungumza kama mtu binafsi bila kuitisha kikao cha Kamati ya Utendaji (EX-COM), na huu ni ukiukwaji wa katiba ya TAHLISO kama chombo chetu. Baada ya EX-COM kukutana kwa dharura kuhusiana na matamko haya ya Mwenyekiti wa TAHLISO, imetafakari kwa kina na kwa kuzingatia katiba ya TAHLSO ikaibaini mapungufu yafuatayo;
1.Ni kwamba mwenzetu huyu amekurupuka katika kutoa matamko haya, tunasema hivi kwa sababu, kwa mujibu wa katiba yetu ya TAHLISO wa Ibara ya 19 inayozungumzia kazi na wajibu wa Katibu Mkuu wa TAHLISO Ikiwa ni pamoja kutoa matamko,taarifa katika vyombo vya habari, mwenyekiti TAHLISO amevunja kipengele hicho na kufanya kazi ambayo si yake kinyume na katiba, kanuni na taratibu za TAHLISO.
2.Mwenzetu huyu ameonyesha ubabaishaji mkubwa kwa kutokuwa makini katika tamko lake kwa kuhusisha Tume ya vyuo vikuu (TCU) na hoja ya upigaji kura kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
Tunasema hivi kwa sababu yeye ni mjumbe wa bodi ya TCU kwa mujibu wa katiba yetu ya TAHLISO, na katika kikao cha TCU kilichofanyika mwezi wa nne ambacho yeye alihudhuria tulitegemea kuwa katika suala hili kama halidhiki nalo angeanza kupinga kwenye kikao kwanza na kama ingeshindikana angekuja kutushawishi sisi wajumbe wa EX-COM kuhusiana na hoja hii ili kama ni maandamano ya amani tuyafanye kipindi hicho.
Hata hivyo wakati tunapokea taarifa ya mjumbe kutoka bodi ya TCU katika mkutano wetu wa senate ambao ulifanyika pale chuo kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA) ndugu Katongo alidiriki kusema hana taarifa yoyote ya kuhusiana na utendaji wa bodi hiyo. Iweje leo aje na kauli hii ya bodi ya TCU kuwa imehusika katika kupanga vyuo vifungue lini ili wanachuo hawa wa elimu ya juu wasipige kura? Kufanya hivi kwanza ni kukiuka msimamo wa bodi hiyo.
Hivi ndugu zangu waandishi wa habari mjumbe akitaka kuzungumzia msimamo wa bodi/kikao cha baraza la mawaziri si lazima ajiuzulu ndipo azungumzie msimamo wa baraza hilo? Si mnakumbuka Mh. Mrema alipotaka kupinga msimamo wa baraza la mawaziri alijiuzuru kwanza ndipo akayazungumzia.
Hivyo basi sababu za wanafunzi kutopiga kura kama alivyobainisha katika tamko lake si za kweli.
Aidha, tunachokiona sisi kama TAHLISO huenda mwenzetu huyu anatumiwa na watu kutufikisha hapa tulipo. Tunasema hivi, Kwa kuwa tunashangaa kwanini hakutuita sisi wenzake EX-COM atueleze haya na tumpe baraka za kuzungumzia haya kikatiba.
3. Kauli ya ndugu Katongo kwamba serikali kwa kuamua vyuo vifunguliwe mwezi Novemba inafanya hivyo kwa makusudi kuwanyima wanafunzi wapatao 60,000 haki yao ya kupiga kura ni kauli isiyo sahihi na ni yenye lengo la kuwapotosha wananchi kwa sababu zifuatazo;
Si kweli kwamba wanavyuo wote wa mwaka 2010/20111 wanapaswa kuwa vyuoni kwa ajili ya kupiga kura.
Mwaka wa kwanza.
Hawa walikuwa form 6 na wengine majumbani, muda wa kujindikisha kupiga kura,hivyo si kweli kwamba wataathirika na zoezi hili maana wao wakati huo hawakuwa wanavyuo. Kitendo cha kuwapeleka vyuoni kabla ya tarehe 31 mwezi Oktoba kupiga kura katika vituo walivyojiandikisha,ni kuwanyima haki yao ya upigaji kura, ambalo tunadhani Ndugu Katongo hakulifanyia utafiti wa kina. Mfano mwaka huu wanafunzi waliodahiliwa kuingia katika vyuo vya elimu ya juu nchini ni zaidi ya wanafunzi 38,000
Mwaka wa tatu.
Wengi wao wamekwisha kumaliza masomo yao ambayo kwa kawaida huishia mwezi julai. Hivyo hata kama vyuo vingefunguliwa mwezi septemba /October wao wasingepaswa kuwa vyuoni wala hawatakatazwa kupiga kura wakiamua.
Mwaka wa pili.
Hawa wengi wao wapo kwenye mazoezi ya vitendo (field) ni suala lao binafsi kwenda chuo na kupiga kura maana hajazuiwa na yeyote na ni utaratibu wa kawaida kila mwaka wao kwenda field. Wengine wapo kwenye mikoa husika hivyo watapiga kura
Kutokana na tukio hilo TAHLISO inatoa taarifa rasmi kama ifuatavyo:-
A. MSIMAMO WA TAHLISO
Umoja huu upo kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya wanafunzi wake wa vyuo vya elimu ya juu nchini Tanzania.
TAHLISO inatambua na kukubaliana kuwa madai yote ambayo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu waliyokuwa wakiyadai kuhusiana na kupata utaratibu wa kupiga kura katika vituo walivyojiandikisha vyuoni ni sahihi na ni halali kabisa na ndiyo maana iliyaanisha na kuyawasilisha serikalini September mwaka huu.
Hata hivyo TAHLISO ni chombo kinachoongozwa kwa kuheshimu maamuzi ya vikao halali katika kuleta umoja na kulinda maslahi ya wanachama wake; kama ilivyoainishwa kwenye katiba kutokana na ukweli TAHLISO haitambui matamko na mipango ya maandamano inayoendelea kufanyika ikiratibiwa na Mwenyekiti Ndg. Katongo, na wala haiamini katika maandamano hayo kwa sasa kutokana na sababu kuu zifuatazo:
1. TAHLISO inaheshimu maamuzi ya vikao halali ambavyo vitafanyika na wanachama wake na vingine ambavyo vimeshafanyika tayari katika kuleta umoja na kulinda maslahi ya wanachama wake kama ilivyoanzishwa kwenye katiba yake (Objectives of TAHLISO ).
Maamuzi aliyoyafanya Ndg. Katongo ya kwenda katika vyombo vya habari na kutangaza maandamano na kuipa serikali saa 48 kutoa majibu kwa TAHLISO yalikwenda kinyume na utaratibu, kanuni na katiba ya TAHLISO kwani kwa mujibu wa katiba ya TAHLISO kiongozi mmoja hana haki ya maamuzi makubwa kuhusu hatma ya WanaTAHLISO bila ya kutumia vikao halali vya TAHLISO.
2. TAHLISO inatamka kwamba maandamano yaliyotangazwa na ndugu Katongo si halali kwa mujibu wa katiba na hatuyaungi mkono kwa kauli moja.
3. TAHLISO ipo kwa ajili kutekeleza majukumu yake kikatiba na si kutumiwa na mtu, au kikundi au chama chochote cha siasa, kwani kwa kufanya hivyo ni kupingana na katiba yetu ya TAHLISO na lengo zima kuanzishwa kwa chombo hiki.
HITIMISHO
TAHLISO inatoa wito kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu nchini Tanzania kutoshiriki maandamano hayo na wapokee fursa yao kikatiba kwenda kupiga kura katika maeneo waliyojiandikisha, bila kushinikizwa na mtu au kikundi chochote kwa manufaa yao binafsi.
Imeandaliwa na
……………………………………
NG’ORO PROSPER GEORGE
KATIBU MKUU TAHLISO
20.10.2010
No comments:
Post a Comment