Tuesday, July 28, 2009


KUTOKA MAGAZETI LEO  

WAFANYAKAZI 600 wa Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena Bandarini (Ticts), jana waligoma kufanya kazi kwa lengo la kuushinikiza uongozi wa kampuni hiyo kutimiza makubaliano sita waliyoafikiana katika mikataba yao ya hiari. 

Pia, walishinikiza kuondolewa kwa Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Neville Bisset na Meneja Utumishi, James Rhombo kwa madai kuwa ndio kikwazo katika kumaliza matatizo yao. 

Wafanyakazi hao walidai kuwa Ticts imeshindwa kutekeleza ahadi ya kuwapandishia ngazi ya mishahara kwa zaidi ya miaka tisa, kuwanyima hisa zao za asilimia tano na kwamba, madereva wa matrekta kufanya kazi kwa zaidi ya saa tisa bila kupata muda wa kula. 

Pia wanapinga kitendo cha wazungu kulipwa fedha nyingi tofauti na wao, kupewa kati ya Sh 5,000 na Sh10,000 kama posho ya ufanyaji kazi katika mazingira magumu kinyume cha makubaliano katika mkataba ambapo walikubaliana kulipwa Sh35,000 na zaidi kwa siku. 

Mbali na posho pia walipinga hatua ya kulipwa Sh75,000 tu badala ya Sh 150,000, inayotokana na upakuaji na upakiaji kwa wastani wa makontena 16 hadi 22 kwa mwezi. 

Dar es Salaam kuanza kuangamiza kunguru weusi 
MKUU wa Mkoa Dar es Salaam, William Lukuvi imewataka wananchi kutoa ushirikiano wa serikali katika kuwaangamiza kungururu weusi waliotapakaa jijini na kuhatarisha maisha ya binadamu na wanyama. 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana alisema kunguru hao ambao awali waliletwa Zanzibar kwa lengo la kula wadudu waliokuwa wanaharibu zao la karafuu visiwani humo; wanazaliana haraka na sasa wanafanya uharibifu katika maeneo mbalimbali. 

Alisema kunguru hao hivi sasa mbali na kusumbua wananchi wanakula ndege wa asili na kuharibu kizazi chao. 

Kwa upande wa binadamu, alisema kunguru hao wanavamia vyakula pamoja na kuharibu mazingira. 

“Kunguru hawa wameshakuwa hatari kwa maisha ya wanyama na binadamu, kwani wamekuwa wakila ndege wetu wa asili na wanaharibu mazingira na mali mbalimbali kikiwemo chakula na makazi ya watu,"alisema Lukuvi. 

Gazeti la Habari Leo : 
Maiti 19 watambuliwa ajali ya Tanga 
Maiti 19 kati ya 28 wa ajali ya basi la Kampuni ya Mohamed Trans lililogongana uso kwa uso na lori katika eneo la Kwakombo wilayani Korogwe mkoani tanga jana wametambuliwa, 14 wamechukuliwa. 

Maiti 27 wamehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, ambapo maiti mmoja anayefanya idadi ya watu waliokufa kuwa 28, alitambuliwa juzi kwenye eneo la tukio na kuchukuliwa. 

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, Dk. Freddy Mtatifikolo, amesema leo kuwa maiti 18 wametambuliwa kwa majina, tisa bado hawajatambuliwa. 

Amesema, kulingana na polisi, abiria waliokuwa wamefunga mikanda ndiyo walionusurika. 

Kati ya walionusurika,wanaume ni 12, wanawake watano na mtoto mmoja wa kike (2), mtanzania mkazi wa Nairobi Kenya . 

Maiti waliochukuliwa hadi leo jioni hospitalini, majina yao na umri ni Hassan Ramadhan (35) wa Manga Handeni, Mkadala Said (32), wa Temeke Dar es Salaam, Ainani Maro (53), Dar es Salaam. 

Mwakyembe ajitoa mhanga, Mongella afyatuka 
Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ameitaka Serikali iufunge mara moja mgodi wa dhahabu wa North Mara ili sumu inayodaiwa kutoka hapo isiendelee kuwadhuru wananchi. 

Mbunge huyo pia ametaka mgodi wa dhahabu wa Geita ufungwe kwa sababu, kwa muda mrefu umekuwa ukitoa kemikali za sumu zinazowadhuru wananchi wa kijiji cha Nyakabale. 

“Kwa nini tuogope wawekezaji kama wakwe” amehoji Mwakyembe na pia kuuuliza kwa nini vifungu vya mikataba havitumiki kuwabana wawekezaji. 

Kwa muda mrefu kumekuwa na madai kuwa mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara umekuwa ikimwaga maji yenye sumu katika mto Tigithe. 

Kwa mujibu wa madai hayo, wananchi 21 kati ya waliyoyatumia maji hayo wamefariki dunia, wengine wamekumbwa na matatizo ya kiafya, na pia mifugo 200 imepoteza maisha. 

Gazeti la Uhuru Leo: 
Benki ya Wanawake kuanza kazi rasmi leo 
SERIKALI imesema kuwa Benki ya Wanawake Tanzania itafungua milango yake na kuanza kazi rasmi leo. 

Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Margaret Sitta, alisema Benki hiyo itaanza kazi katika jengo la Posta ya zamani Jijini Dar es Salaam. 

Alisema tayari mkurugenzi wa kwanza wa Tawi hilo amepatikana na ni mzoefu katika shughuli za kibenki. 

Waziri Margaret alisema benki hiyo itatoa huduma zote za kibenki, na itakuwa wazi kuwahudumia watu wote bila kujali ni wa jinsi gani au dini gani. 

Waziri huyo alisema malengo makuu ya benki hiyo, ni kukusanya amana kutoka kwa wateja, na pia kutoa mikopo ikiwemo ya ujasiriamali, wanaomiliki biashara ndogo, za kati na kubwa. 

Alisema benki hiyo pia itatoa huduma zingine za fedha ikiwemo kubadilisha fedha za kigeni, huduma za kifedha pamoja na kutoa mikopo na ushauri wa masuala ya kibiashara na uzalishaji, hasa kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake. 

Watuhumiwa wa wizi kwa kutumia ATM kizimbani 
RAIA wawili wa Bulgaria wanaotuhumiwa kuiba fedha za wateja wa benki mbalimbali nchini kupitia ATM, wamepandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yanayowakabili. 

Washitakiwa hao, mfanyabiashara Nedko Stanchev (35) na Stela Nedelcheva (23), walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka matatu, baada ya kuahirishwa Alhamisi iliyopita, kutokana na kumkataa mkalimani. 

Upande wa mashitaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Edger Luoga, ulidai mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Warialwande Lema, kuwa mwezi Julai, mwaka huu tarehe na maeneo tofauti mjini Dar es Salaam, walikula njama za kuibia benki ya Barclays sh. milioni 70. 

Katika shitaka la pili, washitakiwa wanadaiwa kughushi ‘VISA CARD’ namba 4205, 6400, 5789, 1838 zilizotolewa kwa Olga Sokolona kuonyesha kwamba zimetolewa kwao na benki hiyo, huku wakijua si kweli. 

Pia Nedko na Stela wanadaiwa kuiba sh. milioni 14.5 mali ya benki ya Barclays kati ya Julai 14 na 17, mwaka huu. Washitakiwa hao wanaotetewa na Wakili Alex Balomi, walikana mashitaka yote. 
  Printable version Email to a friend



No comments:

Post a Comment