Sunday, November 1, 2009


Washindi wa shindano la kusaka wanamuziki wenye kipaji la Bongo Star Search walioingia hatua ya tano bora ya shindano hilo mwaka huu, hatimaye walikabidhiwa zawadi zao za ushindi na kampuni ya Benchmark Production ambao ndio waratibu wa shindano hilo.

Katika shindano hilo ambalo lilifikia kilele siku ya Oktoba 13 washiriki walioingia hatua hiyo ni pamoja na Pascal Cassian, Peter Msechu, Kelvin Mbati, Jackson George, na Beatrice William.

Akizungumza wakati hafla ya kuwakabidhi zawadi zao, Mkurugenzi wa Benchmark Productions, Ritta Paulsen alisema mshindi wa kwanza ambaye ni Cassian amekabidhiwa cheki ya sh milioni 25, wakati wa pili Peter Msechu alipata sh. milioni tano.

Mshindi wa tatu katika shindano hilo, Kelvin Mbati yeye alikabidhiwa fedha taslimu sh milioni tatu, wakati wa Nne ambaye ni Jackson George alipewa sh milioni 1.5, wakati wa tano Beatrice alipata fedha taslimu sh milioni moja.

Ritta alisema washiriki hao wako katika harakati za mwisho za kurekodi albamu yao ya pamoja kwa ajili ya kuitoa kwa jamii.

Naye mshindi wa kwanza katika shindano hilo, Cassian alisema ushindi alioupata ni wa halali kutokana na kura za wananchi walizopiga pamoja na majaji ambao walikuwa wakifuatilia mwanzo mwisho wa shindano hilo.

No comments:

Post a Comment